Monday 31 October 2011

NI MUHIMU KUJUA NYAKATI NA MAJIRA UNAYOISHI - by Azgard Stephen

NI MUHIMU KUJUA NYAKATI NA MAJIRA UNAYOISHI.
Namshukuru Mungu kipekee kwa kunipa nafasi hii ya kukuwekea somo hili. Nasema hivyo kwani inachukua muda kuandaa, ni lazima kuomba ili Mungu anipe ujumbe, lazima nifanye uchunguzi wa kina na pia kuuandika ujumbe katika 'internet'. Kwa hiyo si kazi rahisi, ni lazima kujitoa. Nikuhamasishe tu kwamba, upatapo ujumbe huu, mtumie na mwingine/wengine yeyote ili naye apate hii neema,ili kulijenga kanisa la Kristo.
UTANGULIZI.
Tunapozungumza kwa habari ya nyakati na majira tuna maana hii;
Majira: Ni vipindi mbalimbali ndani ya wakati ulioamriwa; mfano masika, kipupwe, kiangazi, n.k
Nyakati: Ni vipindi kulingana na matukio ya makusudi; mfano asubuhi, jioni, nyakati za mwisho, nyakati za utandawazi, wakati wa kupanda, kuvuna, n.k
Ni muhimu sana kufanya kila jambo kwa wakati na majira yake, mfano kupanda wakati wa kupanda, kuvuna wakati wa kuvuna, n.k
Siku zote ukifanya jambo nje ya wakati wake utaonekana kituko, na matokeo yake ni kutokufanikiwa. Kila jambo huonekana la busara mbele ya wenye hekima likifanyika ndani ya wakati wake, kwa lugha nyingine, "Everything is right at right time". Maana yake ni kwamba ukifanya jambo nje ya wakati hata kama jambo hilo ni jema, litabadilika kuwa baya. Wakati una 'impact' kubwa sana katika jambo lolote. Tazama formula ifuatayo;
1,000,000 * 0 = 0
·  Right thing* Wrong time = Wrong thing
·  Wrong thing * Right time = Right thing
·  Right thing *Right time = Right thing
·  Wrong thing * Wrong time = Wrong thing
Kwa hiyo unaweza kuona ni jinsi gani wakati unavyoweza kuathiri mambo, hii ndiyo 'phylosophy' niliyo nayo. Kwa hiyo jambo ni jema sana likifanywa ndani ya muda wake. Kwa mfano, tendo lile lile linalofanywa na wanandoa likifanywa na watu ambao si wanandoa linakuwa si sahihi. Wala tendo halijabadilika, ni lile lile lakini kwa nini likifanywa na wanandoa ni sahihi na likifanywa na watu ambao si wanandoa sio sahihi? Tena limepewa na jina jingine kabisa, uzinzi; na ukifanya jehanamu unakwenda kwa miguu yote miwili. Tatizo hapa ni wakati!
Mhubiri 3:1-3
Hapa mwandishi anajaribu kutueleza kuwa kila jambo lina wakati na majira yake, tena kila kusudi. Anasisitiza kwa kuonesha mifano kadha wa kadha, wakati wa kuzaliwa, wakati wa kufa, wakati wa kupanda, wakati wa kuvuna n.k.
2Nyakati 1:7-10
Hapa tunamuona Sulemani anafanywa mfalme, akaona hekima na maarifa aliyo nayo hayamtoshi, yalikuwa yanamtosha wakati akiwa kijana, raia wa kawaida; ila wakati huu ni mfalme, hivyo akitazama kazi aliyonayo na kiwango cha hekima na maarifa aliyonayo, haoni uwiano. Mungu anamtokea na kumuuliza, "...omba lolote utakalo nikupe..." Mara Sulemani akakumbuka kiwango chake cha hekima na maarifa wakati huo, akamwambia Mungu, "...nipe sasa hekima na maarifa, nijue kuingia na kutoka mbele ya watu hawa..." Nataka uone jambo hili mahali hapa, si kwamba Sulemani hakuwa na hekima ama maarifa; alikuwa nayo, ila ya kujiongoza mwenyewe. Sasa wakati huu amekuwa mfalme, hivyo anahitaji hekima na maarifa ya kuwaongoza watu wengine.
Daniel 9:2,3
"...mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalitambua hesabu ya miaka, ambayo neno la Mungu lilimjia Yeremia nabii, ya kutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani miaka sabini."
Daniel anaposoma kitabu cha nabii Yeremia anatambua kuwa, wakati waliopo hawapaswi kuwepo Babeli, ila wanatakiwa kuwa wameondoka. Kilichokuwa kimeendelea kuwaweka Babeli ni kutokujua nyakati na majira ambayo wanatakiwa kuondoka Babeli.
Kwa hiyo baada ya Daniel kutambua kuwa walipaswa kukaa Babeli kwa miaka sabini ndipo akamlilia Mungu kumweleza kwamba wanatakiwa waondoke hapo. Kumbe kilichokuwa kinaendelea kuwaweka Babeli ni kutokujua wakati.
1 Nyakati 12:32
"Na wa wana wa Isakari , watu wenye akili za kujua NYAKATI, kuyajua yawapasayo Israel wayatende; ... na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao"
Mungu alijua umuhimu wa watu wa namna hii,watu wanaojua nyakati, kujua wakati gani Israel wanapaswa kufanya nini. Tena Biblia inasema, kwa sababu tu ya wao kujua nyakati, "...ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao". Kwa hiyo ukijua wakati gani unapaswa kufanya nini, utakuwa na ujasiri wa kufanya mambo yako na siku zote utakuwa mtu wa kufanikiwa. Hii ni kwa sababu kila jambo chini ya jua hufanyika ndani ya wakati ulioamriwa, kulingana na mazingira husika. Na ndio maana leo ukikutana na mtu na kumuuliza kwa nini unafanya unachokifanya atakwambia 'nakwenda na wakati'. Ukijua ni wakati gani kitu gani kitatokea utajiandaa kukabiliana nacho.
Mathayo 26:36-46
Yesu alipojua ama alipotambua wakati wa kusulubiwa, alijiandaa kwa kufanya maombi mazito ya kuomba ujasiri wa kukabiliana na hali halisi iliyopo. Kama unafikiri natania, kasome mwenyewe utaona kuna wakati alisema "... kama ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke..." Kwa hiyo maombi aliyokuwa anayafanya, kwa kutambua wakati alionao yalikuwa na umuhimu mkubwa sana, na ni kwa maombi hayo ndipo malaika alishuka akamtia nguvu. Sasa fikiri kama asingejua kuwa huo ndio ulikuwa wakati wa kusulubiwa, halafu asiende kuomba; unafikiri huyo malaika wa kumtia nguvu ama moyo angempata wapi! Ukijua wakati gani unapaswa kufanya nini, utakaa katika eneo husika na utajiandaa kukabiliana na jambo hilo.
Nimekupa dondoo hizo chache za Biblia ili tu uone ni jinsi gani ni muhimu kujua na kutambua nyakati na majira unayoishi.
Nikueleze tu kwamba mafanikio yako ya kiroho na kimwili huendana sana na wakati. Watu hatufanikiwi kwa sababu tu hatujui ni zama gani tunazoishi sasa na tunapaswa kufanya nini. Kwa mfano, kipindi Yesu yuko duniani, yaani karne ya kwanza AD, ilikuwa mtu akiwa na gari linalovutwa na punda, ndiyo alikuwa anaitwa amefanikiwa, ama kwa maneno mengine yeye ni tajiri! Lakini mtu huyo huyo kwa kipindi chetu tunachoishi sasa si tajiri tena kwani mikokoteni ya kuvutwa na punda ni kwa ajili ya kukatia majani ya ng'ombe, kuchotea maji maeneo yenye ukame, kubebea samaki kwa wavuvi, kuzolea takataka kwa maeneo ya mjini, tena uswahilini,n.k. Mafanikio ni yale yale, lakini wakati! Kimsingi kabisa, kinachofanyika leo si kitakachofanyika kesho. Aina ya nyumba anayoishi baba yako leo sio aina ya nyumba utakayoishi wewe! Nizungumze sentensi ngumu kidogo, "kama kipato cha baba yako ni 500,000/= kwa mwezi kwa mfano, na wewe ukaja kuwa na kipato cha 500,000/= kwa mwezi, wewe na baba yako mtakuwa ni wapumbavu!" Sasa unaweza kuniambia kwamba mimi minekutukana,la hasha! Kimsingi ndivyo ilivyo kwani wakati anaoishi baba yako sasa sio wakati utakaoishi wewe, nyakati zinabadilika pamoja na mambo yake yote, hivyo ni muhimu kwa baba yako kukuandaa, na ni muhimu nawe kujiandaa kukabiliana na hali halisi ya wakati huo. Thamani ya pesa itabadilika n.k. Wakati nasoma Galanos, mwalimu wangu mmoja, mtu mzima kidogo, akaniambia kwamba, wakati anaanza kazi ya uwalimu miaka ya sabini, alikuwa analipwa mshahara Tsh. 400/= hivi kwa mwezi, na ni pesa ambayo ilikuwa inamtosheleza kwa mahitaji yake. Lakini kwa sasa analipwa zaidi ya Tsh. 150,000/=. Kazi ni ile ile, lakini mshahara wa wakati ule sio mshahara wa sasa; wakati!
MABADILIKO YA KIUCHUMI NA KISIASA TANZANIA
Miaka ya 1967 - 1985
Ni kipindi ambacho tulikuwa na siasa zaa ujamaa na kujitegemea. Zingatia mambo yafuatayo;
·  Thamani ya fedha ilikuwa juu kuliko sasa. Matumizi ya Tsh. 10/= kwa kipindi kile si kama ilivyo sasa.
·  Matumizi ama mahitaji ya watu yalikuwa chini sana ukilinganisha na sasa kwa sababu ya hali ya maendeleo ilivyokuwa
·  Wasomi walikuwa wachache na kiwango cha elimu kilikuwa chini ukilinganisha na sasa. Mtu wa darasa la saba aliajiliwa na serikali kama mkuu wa mkoa, waziri, n.k. Kwa mfano, waziri wetu mkuu wa kwanza, Kawawa, alikuwa na elimu ya darasa la nne tu, na alipewa jukumu la kuiongoza nchi. Sasa hivi hata kupewa kufagia ofisi za TRA huwezi.
·  Sayansi na Teknolojia ilikuwa chini mno, ni watu wachache mno walikuwa na magari ya kutembelea, computer hazikuwepo, na vitu vingi sana ambavyo unaviona leo.
Pamoja na hayo yote, mafanikio yalikuwepo, walikuwepo watu walioitwa matajiri kwa kipindi hicho, wakati!
Miaka ya 1986 - 1995
Huu ni wakati ambao watu huuita, kipindi cha ruksa. Watu binafsi walikuwa na pesa kuliko serikali. Watu waliacha kazi za kuajiliwa wakafanya biashara. Ilikuwa ni chini ya uongozi wa mzee Mwinyi. Zingatia yafuatayo;
·  Kiwango cha elimu kilianza kupanda, hivyo ajira zikaanza kuwabana watu wa elimu za shule ya msingi
·  Mzunguko wa pesa uliongezeka kwa kiwango cha juu, hivyo kuifanya pesa ianze kushuka thamani. Uchumi ukaanza kukua, watu wakaanza kuwa wamiliki wa mali.
·  Milango ilifunguliwa, bidhaa mbalimbali kutoka nje zikaingia nchini kwa kiwango cha juu kidogo
·  Mabadiliko ya kisiasa yalijitokeza, kulikuwa na mabadiliko kutoka 'monoparty' kwenda kwenye 'multiparty' mwaka 1992, hivyo kubadili kabisa muelekeo wa siasa ya Tanzania.
Miaka ya 1996 - 2005
Huu ni wakati uliopewa majina mengi kidogo, zama za ukweli na uwazi, utandawazi, n.k. chini ya uongozi wa Mh. Mkapa. Zingatia yafuatayo;
·  Mambo yalibadilika kabisa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kwa mara ya kwanza bajeti ya serikali ikagomewa bungeni, wapinzani wote wakatoka bungeni, wabunge wa chama tawala wakaipitisha, mwaka 1996.
·  Mzunguko wa pesa uliongezeka pia kwa kipindi fulani, baadaye ukapungua kwa kuweka 'policies' mbalimbali kama vile 'monetary policy'.
·  Teknolojia imekuwa kwa kasi sana.
·  Kiwango cha elimu kimekuwa, wasomi wameongezeka hivyo kusababisha soko la ajira kuwa gumu.
·  Mawasiliano yamekuwa kwa kiwango cha juu pia.
·  Kumekuwa na uhuru mkubwa wa vyombo vya habari na mawasiliano.
Sasa tuko miaka ya 2006 na kuendelea, chini ya uongozi wa Mh. J.M. Kikwete, mambo yanayoendelea kulingana na zama hizi zinazoitwa zamaa za maisha bora kwa kila Mtanzania wewe ni shahidi, ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya, utakuwa na majibu sahihi kabisa.
Nia na madhumuni ya kukupitisha katika hayo nataka tu uone tunakotoka na tunakokwenda, ili uweze kujua unapaswa kufanya nini. Kulingana na mifano hiyo ningetamani ujifunze mambo yafuatayo;
·  Mabadiliko ya kisiasa yanavyoathiri hali ya maisha ya watu na muelekeo wa nchi, hivyo unapaswa kufanya nini kulingana na hali hiyo. Unaweza kusema kwani siasa zitaniathiri nini, lakini angalia kipindi cha ujamaa, hata kuuza maandazi binafsi ilikuwa hairuhusiwi, kila kitu duka la ushirika, hakukuwa na uhuru wa kutoa maoni kama ilivyo leo, siasa!
·  Mabadiliko ya kiuchumi na jinsi yanavyoathiri maisha ya watu; kwa mfano, kutoka 'socialistic economy' hadi kufikia 'mixed economy'. Ni jinsi gani mabadiliko hayo yameathiri hali ya uchumi ya watu na taifa kwa ujumla. (kumbuka athari zaweza kuwa positive ama negative)
·  Mabadiliko ya sayansi na teknolojia na jinsi yanavyoathiri hali halisi ya maisha ya watu, hivyo ufanye nini.
·  Hali halisi ya kiroho na muelekeo wa kanisa kutokana na mabadiliko hayo, ama kulingana na nyakati zinavyobadilika. Kwa mfano, maadili kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, wewe kama kijana ufanye nini ili kulinda hali yako ya kiroho.
·  Kasi ya maendeleo na mabadiliko hayo, kwa kipindi gani mabadiliko yametokea, na yaliyopo sasa
Nikupashe tu habari kwamba, usitegemee, kwa mfano wewe ni mwanafunzi wa chuo kikuu, hali ya soko la ajira kwa sasa itakuwa hivi hivi hapo wewe utakapomaliza, la hasha! Tazama kitu unachosoma, tazama soko lake kwa sasa, tazama uhitaji (demand) wake kwa sasa, angalia ni wasomi wangapi wako chuo kikuu wanaosomea kitu hicho, tazama idadi ya wale waliopo kazini, angalia kasi ya kukua kwa 'population' mwisho angalia uhitaji (demand) wa kitu hicho kipindi wewe utakapomaliza chuo na miaka utakayokuwa kazini. Unaweza ukasema sasa nitajuaje, nikueleze tu kwamba 'statistics' zipo, tena kwenye internet, hivyo ni wewe tu kuwa makini na kutafuta hayo mambo. Tatizo tulilonalo watanzania ama waafrika kwa ujumla, tunaishi kwa ajili ya leo tu, kesho atajua Mungu. Lakini hiyo sio njia sahihi ya kuishi, na ndio maana Mungu aliweka watu wa kujua mambo yajayo Israel.
Kwa mfano, nchi kama Marekani, wanatengeneza 'computers' ziatakazokidhi mahitaji ya mwaka 2015, yaani wanaitazama 2015 leo kabla hata hawajafika. Wanatazama mfumo wa uchumi wa kipindi hicho leo, wanatazama mahitaji ya watu mwaka 2015 leo. Lakini huku kwetu leo kuna watu wanatumia 'computers' window 2001 na bado hawajamaliza kutumia 'programmes' zilizomo.
Nikueleze tu kwamba, kujua unakoelekea ni muhimu kuliko hata kujiandaa, kwani unaweza ukajiandaa sana, lakini muda ukafika hicho ulichojiandaa hakitumiki tena. Kama unafikiri nakutania, kasomee kutengeneza 'type-writers' sasa hivi, halafu uwe unategemea kuja kufanya kazi kama 'engineer', yaani kukamilisha masomo yako mwaka 2020 uone kitakachokutokea. Nasisitiza kwamba, ni muhimu sana kuangalia soko la kile kitu unachofanya leo kwa miaka utakayokuja kukifanyia kazi, ni muhimu sana. Kwa mfano, kwa sasa kuna wanafunzi wengi sana wanasoma sheria, wengi mno. Lakini mimi nikiangalia tunakokwenda, soko la ajira katika sheria na wanafunzi walioko vyuoni hakuna uwiano, hivyo ni dhahiri kwamba kuna watu wengi sana, wasomi, ajira itakuja kuwa kitendawili kwao, hivyo itawapasa kuja kujiajiri wenyewe. Sasa kujiajiri mwenyewe si tatizo, tena ni jambo jema sana, lakini je huyu mtu amejiandaa kujiajiri? Maana kitakachotokea ni maandamano, ajira hakuna! Sasa sikukatishi tamaa usisome sheria, ila nataka tu uone unakoelekea na ujiandae kukabiliana na hali utakayoikuta huko.
Kuna watu wanafanya mambo siku za leo wakidai wanakwenda na wakati, lakini kimsingi hawaendi na wakati ila wanafanya mambo yaliyopitwa na wakati. Kwa mfano, siku moja muinjilisti mmoja alikuwa nahubiri, akawauliza wakina dada kwa nini wanapakaa wanja; wenyewe wakadai wanakwenda na wakati. Yule muinjilisti kawaambia, "Mngejua kwamba huyo aliyeanza kupaka wanja alifanya hivyo miaka 700 kabla ya Kristo, na alikuwa ni Yezebeli, mke wa Ahabu, ambaye alikuwa mwanzilishi wa mungu Baali, na anaitwa mama wa makahaba, msingepaka wanja kwa kudai mnakwenda na wakati!" Nimekupa tu 'challenge' ujue ukifanya kitu unakifanya kwa misingi gani. Sasa sikwambii usipake wanja, hasha! ila tu ni muhimu kujua kwa nini unapaka wanja!
Kama Mungu akinipa nguvu, nitakutumia mfululizo wa pili wa somo hili unaohusu nyakati za mwisho, yaani kurudi kwa Masihi kulichukua kanisa na kitu gani kitajili baada ya hapo. Usikose kufuatilia. Kama nikisahau, nikumbushe, ama fuatilia katika e-mail hii, watumishi07@yahoo.com kwa kutumia password hii maombi. Neema ya Mungu ikufunike na Roho mtakatifu akuwezeshe kuyaelewa haya.
Ev. Azgard S.Chamulungwana
sheghwede@yahoo.com
+255713990607

Monday 17 October 2011

KARIBUNI SANA UDOM FIRST YEAR 2011/2012

CHRISTIAN FELLOWSHIP - UNIVERSITY OF DODOMA INAWAKARIBISHA SANA WAPENDWA WOTE MWAKA WA KWANZA KATIKA CHUO KIKUU CHA DODOMA, NA HASA KUABUDU PAMOJA CHRISTIAN FELLOWSHIP. TAARIFA ZA MAHALI PA KUABUDU SIKU ZA KATI ZA WIKI MTAZIPATA KWA MWENYEKITI BARAKA #0769107000, NA KUPITIA MATANGAZO KWA NJIA MBALIMBALI...KARIBUNI SANA TUABUDU KWA PAMOJA

KURUDI KWA MASIHI NA DALILI ZAKE

Namshukuru Mungu kwa mara nyingine tena kukuletea mfululizo wa pili wa somo la 'NI MUHIMU KUJUA MAJIRA NA NYAKATI UNAZOISHI'. Ni matumaini yangu kuwa kama unafuatilia vizuri masomo ninayokutumia unabarikiwa na unajifunza kitu kwa namna moja ama nyingine. Sasa naomba jifunze sehemu hii ya pili ambayo nimelenga kukueleza machache tu kwa habari ya kurudi kwa Bwana Yesu kulichukua kanisa, dalili zake na mambo yatakayojili baada ya hapo.
Nikueleze tu kwamba siku za mwisho zilianza mara tu baada ya Yesu kupaa.
Yesu hakuweka wazi kuwa ni lini atarudi kulichukuwa kanisa, lakini aliweka wazi mambo kadha wa kadha juu ya kuja kwake. Alisema katika Mathayo 24:36, kwa habari ya siku ya kurudi hata malaika hawajui ila baba mwenyewe.
Mathayo 24.
Kitabu hiki kinaeleza kwa ufupi, ila kwa umakini wa hali ya juu sana kwa kile kitakachotokea. Nia na madhumuni ya kitabu hiki ni kukujulisha kwa habari za siku za mwisho, dalili zake na kurudi kwa masihi wa Bwana. Maana yake ni kwamba matukio ndiyo yatakayoeleza nyakati. Natamani uone jambo hili kwamba majira na nyakati za kurudi kwa Bwana huelezwa na matukio yanayojili, na ndio maana kila wakati Yesu alisema, "...mkiona...mjue..." Sasa naamini unaelewa namaanisha nini. Natamani sasa niweke kile kitakachotokea kwa mfululizo wake, moja baada ya jingine;
Kupaa kwa Bwana Yesu kwenda mbinguni.
·  Jambo hili lilishatokea tayari, hata wewe ni shahidi wa hili na ndio maana umeokoka unasubiri kwenda mbinguni. Soma Mdo 1:9-11; Luka 24:51; Marko 16:19
Dalili za siku za mwisho.
·  Kubomolewa kwa hekalu: Yesu alisema katika Mathayo 24:2, "...amin, amin nawaambieni, halitasalia hapa jiwe ambalo halitabomoshwa". Hii ni baada ya wanafunzi wake kumuonesha mawe ya hekalu na misingi yake ilivyo imara.Hekalu lilikuja kubomolewa miaka 70 AD. Na sasa eneo hilo lilipokuwepo hekalu limejengwa msikiti.
·  Dalili nyingine nyingi: Soma hiyo mathayo kuanzia mst wa 4 utaona dalili nyingi ambazo nyingi zimeshatimia hadi sasa; mfano, vita, matetemeko ya ardhi, magonjwa ya kutisha, maarifa kuongezeka (angalia teknolojia ilivyo juu sasa hivi), n.k
Kurudi kwa Yesu mara ya pili (unyakuo).
Hili ndilo subirio kubwa la watakatifu wa Mungu. Siku moja nikawaambia watu kwamba kama mimi ningeulizwa Yesu arudi sasa ama la, ningesema asirudi kwanza, watu walinishangaa, labda na wengine kuniona natania. Pengine nawe waweza kunishangaa, lakini ngoja nikwambie, nilisema hivyo kwani nilikuwa nikiangalia kiwango nilichotumika, nikaona bado sijafanya kazi ya kuridhisha. Sijafika sehemu ya kusimama kama Paulo na kusema, "...kazi nimeimaliza, vita nimevipiga, imani nimeilinda..." Nasema hivyo kwani tukifika mbinguni tutapewa taji, na 'size' ya taji itategemea kazi uliyofanya! Sasa nafikiri unaelewa kwa nini nilisema vile.
·  Mathayo 24:27,28,40,41. "Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adamu. Kwa kuwa popote ulipo mzoga ndipo wakutanikapo tai...Wakati ule watu wawili watakuwepo kondeni, mmoja atwaliwa mmoja aachwa;wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa."
·  1 Thesalonike 4:16,17. "Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele..."
·  1Kor 15:52,53. "Kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uhalibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti huu (mwili) uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa." Ieleweke kwamba wakati parapanda itakapolia, wafu waliolala katika Kristo, yaani waliookoka peke yao ndio watakaofufuka. Watakaomwona Kristo kwa wakati huu ni watakatifu peke yao. Kristo hataigusa ardhi kwa wakati huu, na badala yake tutamlaki mawinguni. Shughuli za dunia hii zitaendelea kama kawaida. Pia uelewe kwamba mbinguni hatutakaa milele. Huko tutaimba wimbo wa mwana-kondoo, tutakula karamu ya mwana-kondoo na kuvikwa taji za ushindi, KWA KADRI YA KAZI TULIZOFANYA. Tutakaa huko kwa miaka saba kisha tutashuka duniani na Bwana (Nitatoa somo hili la 'badget' ya miaka kulingana na matukio kwa kutumia kitabu cha Daniel 9:24-27) na ndipo tutatawala na Bwana kwa miaka elfu duniani.
Dhiki kuu.
·  Jambo hili, niaminivyo mimi kulingana na maandiko, litatokea huku duniani wakati sisi watakatifu tukiwa mbinguni. Huu ndio wakati ambao mpinga Kristo atafanya kazi. Kinachomzuia sasa ni kanisa. 2Thes 2:6,7. "Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa kwa wakati wake. Maana ile siri ya kuasi sasa inatenda kazi; lakini yupo azuiaye(kanisa) sasa, hata atakapoondolewa."
·  Ukisoma kitabu cha ufunuo kuanzia sura ya nne utaelewa ninachosema. Ile sura ya tisa anaeleza baadhi tu ya dhiki hizo.
·  Chapa ya mpinga Kristo itafanyakazi wakati huu. Ufunuo 13:18. "Yeye mwenye akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita."
·  Wengi watakufa kwa makali ya upanga. Lakini pia watu watatafuta mauti, haitakuwepo. Yaani mtu anatafuta kufa lakini hafi! Ufunuo 9:5,6. "Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe kwa miezi mitano...Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, mauti itawakimbia."
·  Hii dhiki ni kubwa,kila atakayekuwepo atajuta kuwepo. Niliposoma kitabu hiki cha ufunuo nilishangaa, kuna watakatifu(waliookoka) watakuwepo. Nikajiuliuza kwa nini; lakini kumbe ni wale ambao hawakutenda kazi; yaani walikuwepo tu duniani wakisubiri kwenda mbinguni. Wakati mbinguni tunakwenda kupewa taji za kazi tulizofanya, wao hawakufanya kazi.
kurudi kwa Yesu mara ya tatu.
·  Hapa tutarudi ama tutashuka pamoja na Bwana tukitokea mbinguni, tukiwa tumevaa taji zetu za ushindi. Tutakuja kuitawala dunia. Mathayo 24:30,31 anasema, "...ndipo itakapoonekana ishara yake mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza nao watamwona mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi." Kumbuka pale mwanzoni, akija mwana wa Adamu mara ya pili, watakatifu watamlaki mawinguni wakishangilia na kuondoka naye; hapa anasema anakuja na utukufu mwingi, badala ya watu kushangilia na kuondoka naye, wanaomboleza!
·  Hapa ndipo pale Paulo anasema, kila jicho litamwona! Si kama mkombozi tena, ila kama mtawala, hakimu n.k.
·  Tutakaa pamoja naye katika mlima wa mizeituni kule Israel, yaani pale ndipo itakapokuwepo Ikulu ya ufalme huo. Tena Biblia inasema itakuwepo kambi ama ngome ya watakatifu.
Kutawala na Bwana miaka elfu (Millenium of Peace) Ufunuo 20:1-6
·  Tutawala na Kristo, shetani atafungwa kipindi chote hiki cha miaka 1000, mpinga Kristo atatupwa Jehanamu ya moto, pamoja na yule nabii wa uongo (kumbuka hawa watakuwa wanadamu wa kawaida tu, yaani mpinga Kristo na nabii wa uongo).
·  Utakuwa ni wakati wa amani mno, nabii Isaya anasema, "...mwana-simba atacheza na mwana-kondoo..."
·  Ufunuo 20:5,6. "Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa ukuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu."
Hukumu ya mwisho (The last judgement) Ufunuo 20:11-15
"Nikaona wafu wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawa sawa na matendo yao...na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto."
·  Hapa ni baada ya ile miaka elfu, wale ambao hawakufufuka bado, yaani walikufa katika dhambi, watafufuliwa hapa ili wasomewe hukumu zao.
·  Hukumu hii ni ukomo wa mambo ya zamani, mara baada ya hapo tutaanza kuona mambo mapya kabisa.
Mbingu mpya na nchi mpya. Ufunuo 21:1-7
"Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi za kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari...Tazama maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao,nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao...Tazama nayafanya yote kuwa mapya...Yeye ashindaye atayarithi haya, mimi nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu."
·  Huu ndio mwisho uliokuwa ukisubiriwa kwa zaidi ya miaka 1000 baada ya unyakuo. Hapa ndipo tutaishi milele na milele.
·  Huu mji mpya, Yerusalemu una sifa nyingi ambazo kwa namna ya kawaida hazielezeki, kila nikipiga picha, kila siku napata picha mpya. Njia zake ni dhahabu tupu, milango yake ni lulu safi, n.k. Soma mwenyewe Ufunuo 21:9-27.
·  Biblia haisemi baada ya sisi kuingia mji huo utapaa kuelekea mbinguni kama ulivyoshuka, ila inasema tutaishi humo, tena tukiingia na kutoka kwani milango yake haitafungwa daima.
·  Nionavyo mimi, wala si Roho sasa, ni mawazo na maoni yangu mimi, kwamba hatutaondoka kwenda mbinguni tena, ila tutakaa humo tukiingia na kutoka, yaani tutakuwa tukingia na kutoka ndani ya mji, ili kufurahia mji pamoja na hii mbingu na nchi mpya ambazo Mungu amezitengeneza. Maana kama tutaondoka tena, hii nchi mpya nani atakaa? Nawe waweza kuwa na mawazo yako. Biblia inasema tunajua kwa sehemu tu.
Nimalize kwa kukupa angalizo kwamba, kuna 'doctrines' nyingi sana kwa habari ya siku za mwisho, hivyo kile ninachokuletea ni kile ninachoamini mimi. Huwa napenda kuwaambia watu kwamba, ni muhimu sana kuweka machujio (filters) ya kiroho, kuchuja kila unachopokea, kwa kutumia maandiko na Roho mtakatifu ndani yako na ndipo uamini kwani kuna mafunuo mengi mno katika siku tunazoishi leo, hivyo kuwa makini!
Lakini pia, jiweke tayari muda wowote, ufaao na usiofaa, kwani huwezi kujua ni lini na saa ngapi Bwana wetu atarudi. Paulo alisema, "...tusije tukawa watu wa kukataliwa siku ile..."
Basi neema ya Kristo na ikutunze, zaidi sana Roho mtakatifu akuwezeshe kuyaelewa haya. Usisahau kuwatumia wengine. Ukilichukulia hilo kama wajibu, kwa namna ile ile mimi nilivyolichukulia kama wajibu wangu kukutumia wewe, tutafanikisha pamoja kuujenga mwili wa Kristo.
Kwa maswali,ushauri ama mawasiliano ya namna yoyote ile na saa yoyoye,
Ev. Azgard S. Chamulungwana
sheghwede@yahoo.com
+255713990607