ALIPOANZA SHULE YA MSINGI RUNGWE
.
BAHATI BUKUKU
MWAKA 1988, RUNGWE, MBEYA
“Lusako amka...Lusako amka, niliisikia sauti ya baba
yangu, mzee John Bukuku akiniamsha asubuhi sana tofauti na siku nyingine.
“Lusako ni jina langu lingine ambalo kwetu lina maana ya ‘ngekewa’ au ‘bahati’.
“Siku ile baba alinitaka niamke kwa ajili ya kujiandaa na kwenda kuanza darasa
la kwanza katika Shule ya Msingi iitwayo Muungano iliyopo Ilolo, Mbeya.
“Nilikurupuka kutoka kitandani, nilikuwa mdogo mno, miaka saba tu. Baada ya
kuisikia sauti ya baba yangu, nikaamka na kutoka nje. “Naikumbuka siku hii
vilivyo kwa sababu ndiyo ilikuwa siku niliyokuwa nikiisubiria kwa hamu kubwa.
“Kila siku nilikuwa nikiwaona watoto wenzangu wakienda shule, walivalia sare
zao za shule huku wakiwa na madaftari. Nilitamani sana kuwa kama wao.
Nilitamani nami siku moja nibebe madaftari yangu, nivae sare za shule na
kuelekea shuleni kusoma.
“Ukiachana na watoto hao waliokuwa wakipita nyumbani
kuelekea kwetu shuleni, dada yangu aliyeitwa Selina alikuwa akiniambia mambo
mengi kuhusu shule, hasa kunywa uji mwingi wenye sukari, nami nikajikuta
nikianza kutamani kusoma. “Kila nilipokuwa nikikaa, nilitamani siku ifike na
mimi nivae sare za shule na kuelekea shuleni. Siku niliziona haziendi, kiu
kubwa ya kutamani kusoma ilinishika. “Kila nilipokuwa nikimsikilizia baba kuona
kama alikuwa akitaka kunipeleka shule, hakuwa akifanya hivyo. Niliumia sana
moyoni. “Siku hiyo ambayo baba alikuwa ameniamsha. Nilijiandaa tayari kwa
kwenda shule kwani niliamini kwamba siku hiyo ndiyo ingekuwa siku ya kwanza
kwangu kuanza masomo shuleni. “Nikajiandaa huku mama akinivaliasha nguo safi,
baba akanishika mkono na kuanza kwenda shule. “Njia nzima, nilijisikia furaha
isiyo kifani, kitendo cha kupelekwa shule siku hiyo kilinifanya kujisikia mtu
wa tofauti sana, furaha ilinizidi hadi nikaona tulikuwa tukichelewa kufika
shule.
Nilitaka na mimi nikae darasani na kuanza kusoma. “Kwa sababu shule
haikuwa mbali sana, tulichukua dakika chache tukafika. Sikuwa peke yangu, bali
kulikuwa na watoto wengi ambao waliletwa shuleni hapo na wazazi wao kwa ajili
ya kuanza darasa la kwanza katika shule hiyo ya Muungano iliyokuwa mita mia
moja na ishirini kutoka nyumbani kwetu. “Kila mtoto aliyeletwa shuleni hapo
alionekana kuwa na furaha, kitendo cha kuitwa kwa ajili ya kuanza masomo
kilimfurahisha kila mmoja na kuamini kwamba ilikuwa ni lazima tuanze masomo ili
na sisi tuanze kuvaa sare na hata kunywa uji kila tufikapo shuleni hapo.
“Staili ya zamani ya kuchagua wanafunzi wa kujiunga na darasa la kwanza ilikuwa
tofauti. Watoto wote walioletwa shuleni hapo, walitakiwa kusimama na kuupitisha
mkono wao kichwani ili kushika sikio la upande wa pili. “Endapo mtoto angeweza
kushika sikio, basi alikuwa amefaulu kuanza darasa la kwanza lakini kama
alifeli, basi hakutakiwa kuanza shule. “Baada ya kuona baadhi ya watoto
wenzangu wameshindwa kulishika sikio, nikahofia kwa kuona kwamba hata mimi pia
ningeshindwa, hivyo nikaanza kujipa mazoezi, kila nilipopitisha mkono,
nilishindwa kulishika sikio langu. “Hapo, tayari nikaona kwamba ningeshindwa
kuanza masomo yangu, nilichokifanya ni kung’ang’ania kutaka kulishika sikio
lile ili ikiwezekana, nilishike tu kisha nimfuate mwalimu huku mkono wangu
ukiwa sikioni. “Bahati mbaya nilishindwa kufanya hivyo. “Zamu yangu ilipofika,
nikaambiwa niupitishe mkono wangu kichwani na kulishika sikio la upande wa
pili, nikashindwa na hivyo mwalimu kusema kwamba sikutakiwa kuanza darasa la
kwanza.Nilitakiwa nirudi nyumbani hadi mwaka unaofuata.
HISTORIA
YA MAISHA YA BAHATI BUKUKU (Sehemu ya 2)
Bahati Bukuku. Nilipenda kwenda shule
kusoma, na hii ilikuwa njia mojawapo ya kuepuka kufanya kazi za nyumbani, hasa
kuosha vyombo kitu nilichokuwa nikikichukia mno. Japokuwa nilikuwa mtoto mdogo
lakini mama alijitahidi sana kuniweka katika mazingira ambayo mtoto wa kike
anatakiwa kuwa. Achukia kuosha vyombo Kila siku alikuwa akinitaka nioshe
vyombo, hii ilikuwa kazi pekee niliyokuwa nikiichukia mno. Kila nilipokuwa
nikirudi nyumbani, mama alikuwa akinipa maziwa na kiporo cha jana, nikimaliza
kula, alikuwa akiniambia nioshe vyombo nilivyovitumia. Nilikereka mno lakini
sikuwa na jinsi, nilibaki nikilalamikalalamika lakini mwisho wa siku niliosha
vyombo mbele yake huku akionekana kuwa na furaha.
AWA KIONGOZI WA KUIMBA
Ijulikane kwamba kuimba ni kipaji nilichozaliwa nacho. Nakumbuka kipindi hicho mimi
ndiye nilikuwa kiongozi wa nyimbo mbalimbali tulizokuwa tukiimba shuleni. Sauti
yangu haikuwa nzuri, ilikuwa ni ya kukoroma sana lakini kila nilipokuwa
nikiimba walimu waliipenda na ilikuwa ni lazima ujue kwamba ‘huyo anayeimba ni
Lusako’.
AANZA DARASA LA KWANZA
Baada ya kusoma shule ya chekechea kwa miaka
miwili, mwaka 1990 nilitakiwa kwenda kuanza darasa la kwanza katika Shule ya
Msingi Muungano ambayo haikuwa mbali kutoka tulipokuwa tukiishi. Kama kawaida
yangu, siku hiyo niliamka asubuhi sana huku nikiwa na hamu ya kuanza darasa la
kwanza. Moyo wangu haukuweza kusahau, bado niliendelea kukumbuka miaka miwili
iliyopita ambapo nilishindwa kulishika sikio langu la upande wa kushoto kwa
kutumia mkono wangu wa kulia kwa kuupitisha kichwani. Kwanza kabla ya yote,
hapohapo nyumbani, nikajaribu kulishika sikio langu, nikafanikiwa.
ACHEKELEA
KUJIUNGA NA SHULE YA MSINGI
Naweza kusema kwamba katika mwaka huo, siku hiyo
ndiyo nilikuwa na furaha kupita kawaida. Nilipenda sana shule, kila nilipokuwa
nikiwaona wanafunzi wakipita nyumbani huku wakiwa wamevalia sare zao za shule,
niliona wivu moyoni. Leo hii na mimi nilitakiwa kwenda kuanza darasa la kwanza!
Asubuhi ya siku hiyo, mama akaniletea sketi na shati huku chini nikivalia soksi
za pundamilia. Sikuwa na sare za shule hivyo siku hiyo nilivalia nguo za
nyumbani ila miguuni nilikuwa na soksi hizo za pundamilia. Baada ya kutembea
kwa umbali mdogo, nikaelekea shuleni huku nikiongozana na baba, mzee Bukuku.
Watoto waliokuja kuanza shule walikuwa wengi na zoezi lilikuwa lilelile la
miaka yote, kushika sikio lako. Wapo walioshindwa ambao walilia kama
nilivyofanya miaka miwili iliyopita lakini pia walikuwepo wale waliofaulu na
kutakiwa kujiunga na shule hiyo kwa ajili ya kuanza na elimu ya msingi huku
nikiwa nimeandikishwa jina jingine na kuitwa Bahati.
AANZA MASOMO
Niliipenda
masomo, niliipenda shule kwa jinsi majengo yake yalivyokuwa. Yalipendeza na
kuvutia sana. Siku hiyohiyo ambayo baba alikuwa amenipeleka shuleni hapo,
tukaingizwa darasani na kupangwa, siku iliyofuata, tukaanza masomo huku tukiwa
watoto zaidi ya arobaini katika darasa moja. Kila mmoja alionekana kuwa na
furaha kama nilivyokuwa. Hakukuwa na utulivu, kila wakati wanafunzi walikuwa
wakipiga kelele, nadhani kwa walimu au kwa watu waliokuwa katika mitaa yenye
watoto wengi watakuwa wanalitambua hili, jinsi watoto wanavyopiga kelele zenye
kuleta kero.
AONGOZA KWA UTUNDU
Kati ya wanafunzi wote waliokuwa darasani, mimi
ndiye nilionekana kuwa mtundu. Kwanza sikutulia sehemu moja, nilionekana kama
mtu aliyekuwa akitafuta kitu fulani, muda huu unaweza kuniona hapa na baadaye
kuniona kule.
UTUNDU WAMPA UMONITA
Kutokana na utundu wangu wa muda mfupi, hata
mwalimu wa darasa hilo aitwaye Rugemilila alipoingia darasani, akanichagua niwe
‘monita’ yaani kiongozi wa darasa lile. Maisha ya nyumbani yaliendelea kuwa
vilevile kwamba kila nilipokuwa nikirudi na kula chakula, mama alinitaka nioshe
vyombo. Bado mama alinifundisha mambo mengi huku akitamani sana niwe kama
wasichana wengine, nadhani mbele ya maisha yangu aliyaona kwani kwa kile
alichokuwa akikitaka ndicho kimeweza kunisaidia sana kipindi hiki.
AKAMUA
NG’OMBE MAZIWA
Kazi zote za nyumbani ambazo alikuwa akizifanya mama, ilikuwa ni
lazima na mimi nizifanye. Siku ambayo sikuwa nikienda shule, ilikuwa ni lazima
nipike japo chai na kufanya usafi nyumbani hapo huku nikisaidiana naye.
Nyumbani kulikuwa na ng’ombe, kila siku, hata kabla ya kwenda shule ilikuwa ni
lazima niamke asubuhi sana, nikamue maziwa na kisha mtu ambaye alikuwa
akihusika kwa ajili ya kwenda kuwachunga akiwatoa zizini na kwenda nao
machungoni.
ACHUNGA NG’OMBE
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu ya kila siku. Siku
ambazo sikuwa nikielekea shuleni, pia nilikuwa nikichukuliwa na kupelekwa
machungoni. Nilichukia kazi nyingine lakini hii ya kuwapeleka ng’ombe machungoni
niliipenda kwa sababu ilinipa nafasi ya kuondoka nyumbani hapo kwenda kuzurura
na ng’ombe hao.
AUZA CHIPSI
Kutokana na utundu niliokuwa nao na ujanja wa hapa
na pale, mwalimu wangu wa darasa akanichagua niuze chipsi zake. Wanafunzi wengi
walikuwa wakiitamani kazi hii kwani walijua fika kwamba mara unapouza na
nyingine kubaki, walimu huwa na kawaida ya kukupa mfuko mmoja ule.
Chanzo-globalpublishers