Thursday 27 November 2014

HISTORIA YA MAISHA YA BAHATI BUKUKU

ALIPOANZA SHULE YA MSINGI RUNGWE
BAHATI BUKUKU MWAKA 1988, RUNGWE, MBEYA 
 



“Lusako amka...Lusako amka, niliisikia sauti ya baba yangu, mzee John Bukuku akiniamsha asubuhi sana tofauti na siku nyingine. “Lusako ni jina langu lingine ambalo kwetu lina maana ya ‘ngekewa’ au ‘bahati’. “Siku ile baba alinitaka niamke kwa ajili ya kujiandaa na kwenda kuanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi iitwayo Muungano iliyopo Ilolo, Mbeya. “Nilikurupuka kutoka kitandani, nilikuwa mdogo mno, miaka saba tu. Baada ya kuisikia sauti ya baba yangu, nikaamka na kutoka nje. “Naikumbuka siku hii vilivyo kwa sababu ndiyo ilikuwa siku niliyokuwa nikiisubiria kwa hamu kubwa. “Kila siku nilikuwa nikiwaona watoto wenzangu wakienda shule, walivalia sare zao za shule huku wakiwa na madaftari. Nilitamani sana kuwa kama wao. Nilitamani nami siku moja nibebe madaftari yangu, nivae sare za shule na kuelekea shuleni kusoma.

 “Ukiachana na watoto hao waliokuwa wakipita nyumbani kuelekea kwetu shuleni, dada yangu aliyeitwa Selina alikuwa akiniambia mambo mengi kuhusu shule, hasa kunywa uji mwingi wenye sukari, nami nikajikuta nikianza kutamani kusoma. “Kila nilipokuwa nikikaa, nilitamani siku ifike na mimi nivae sare za shule na kuelekea shuleni. Siku niliziona haziendi, kiu kubwa ya kutamani kusoma ilinishika. “Kila nilipokuwa nikimsikilizia baba kuona kama alikuwa akitaka kunipeleka shule, hakuwa akifanya hivyo. Niliumia sana moyoni. “Siku hiyo ambayo baba alikuwa ameniamsha. Nilijiandaa tayari kwa kwenda shule kwani niliamini kwamba siku hiyo ndiyo ingekuwa siku ya kwanza kwangu kuanza masomo shuleni. “Nikajiandaa huku mama akinivaliasha nguo safi, baba akanishika mkono na kuanza kwenda shule. “Njia nzima, nilijisikia furaha isiyo kifani, kitendo cha kupelekwa shule siku hiyo kilinifanya kujisikia mtu wa tofauti sana, furaha ilinizidi hadi nikaona tulikuwa tukichelewa kufika shule.

 Nilitaka na mimi nikae darasani na kuanza kusoma. “Kwa sababu shule haikuwa mbali sana, tulichukua dakika chache tukafika. Sikuwa peke yangu, bali kulikuwa na watoto wengi ambao waliletwa shuleni hapo na wazazi wao kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza katika shule hiyo ya Muungano iliyokuwa mita mia moja na ishirini kutoka nyumbani kwetu. “Kila mtoto aliyeletwa shuleni hapo alionekana kuwa na furaha, kitendo cha kuitwa kwa ajili ya kuanza masomo kilimfurahisha kila mmoja na kuamini kwamba ilikuwa ni lazima tuanze masomo ili na sisi tuanze kuvaa sare na hata kunywa uji kila tufikapo shuleni hapo.


 “Staili ya zamani ya kuchagua wanafunzi wa kujiunga na darasa la kwanza ilikuwa tofauti. Watoto wote walioletwa shuleni hapo, walitakiwa kusimama na kuupitisha mkono wao kichwani ili kushika sikio la upande wa pili. “Endapo mtoto angeweza kushika sikio, basi alikuwa amefaulu kuanza darasa la kwanza lakini kama alifeli, basi hakutakiwa kuanza shule. “Baada ya kuona baadhi ya watoto wenzangu wameshindwa kulishika sikio, nikahofia kwa kuona kwamba hata mimi pia ningeshindwa, hivyo nikaanza kujipa mazoezi, kila nilipopitisha mkono, nilishindwa kulishika sikio langu. “Hapo, tayari nikaona kwamba ningeshindwa kuanza masomo yangu, nilichokifanya ni kung’ang’ania kutaka kulishika sikio lile ili ikiwezekana, nilishike tu kisha nimfuate mwalimu huku mkono wangu ukiwa sikioni. “Bahati mbaya nilishindwa kufanya hivyo. “Zamu yangu ilipofika, nikaambiwa niupitishe mkono wangu kichwani na kulishika sikio la upande wa pili, nikashindwa na hivyo mwalimu kusema kwamba sikutakiwa kuanza darasa la kwanza.Nilitakiwa nirudi nyumbani hadi mwaka unaofuata.


HISTORIA YA MAISHA YA BAHATI BUKUKU (Sehemu ya 2)
 Bahati Bukuku. Nilipenda kwenda shule kusoma, na hii ilikuwa njia mojawapo ya kuepuka kufanya kazi za nyumbani, hasa kuosha vyombo kitu nilichokuwa nikikichukia mno. Japokuwa nilikuwa mtoto mdogo lakini mama alijitahidi sana kuniweka katika mazingira ambayo mtoto wa kike anatakiwa kuwa. Achukia kuosha vyombo Kila siku alikuwa akinitaka nioshe vyombo, hii ilikuwa kazi pekee niliyokuwa nikiichukia mno. Kila nilipokuwa nikirudi nyumbani, mama alikuwa akinipa maziwa na kiporo cha jana, nikimaliza kula, alikuwa akiniambia nioshe vyombo nilivyovitumia. Nilikereka mno lakini sikuwa na jinsi, nilibaki nikilalamikalalamika lakini mwisho wa siku niliosha vyombo mbele yake huku akionekana kuwa na furaha.
 AWA KIONGOZI WA KUIMBA 
Ijulikane kwamba kuimba ni kipaji nilichozaliwa nacho. Nakumbuka kipindi hicho mimi ndiye nilikuwa kiongozi wa nyimbo mbalimbali tulizokuwa tukiimba shuleni. Sauti yangu haikuwa nzuri, ilikuwa ni ya kukoroma sana lakini kila nilipokuwa nikiimba walimu waliipenda na ilikuwa ni lazima ujue kwamba ‘huyo anayeimba ni Lusako’.
 AANZA DARASA LA KWANZA 
Baada ya kusoma shule ya chekechea kwa miaka miwili, mwaka 1990 nilitakiwa kwenda kuanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Muungano ambayo haikuwa mbali kutoka tulipokuwa tukiishi. Kama kawaida yangu, siku hiyo niliamka asubuhi sana huku nikiwa na hamu ya kuanza darasa la kwanza. Moyo wangu haukuweza kusahau, bado niliendelea kukumbuka miaka miwili iliyopita ambapo nilishindwa kulishika sikio langu la upande wa kushoto kwa kutumia mkono wangu wa kulia kwa kuupitisha kichwani. Kwanza kabla ya yote, hapohapo nyumbani, nikajaribu kulishika sikio langu, nikafanikiwa. 
ACHEKELEA KUJIUNGA NA SHULE YA MSINGI 
Naweza kusema kwamba katika mwaka huo, siku hiyo ndiyo nilikuwa na furaha kupita kawaida. Nilipenda sana shule, kila nilipokuwa nikiwaona wanafunzi wakipita nyumbani huku wakiwa wamevalia sare zao za shule, niliona wivu moyoni. Leo hii na mimi nilitakiwa kwenda kuanza darasa la kwanza! Asubuhi ya siku hiyo, mama akaniletea sketi na shati huku chini nikivalia soksi za pundamilia. Sikuwa na sare za shule hivyo siku hiyo nilivalia nguo za nyumbani ila miguuni nilikuwa na soksi hizo za pundamilia. Baada ya kutembea kwa umbali mdogo, nikaelekea shuleni huku nikiongozana na baba, mzee Bukuku. Watoto waliokuja kuanza shule walikuwa wengi na zoezi lilikuwa lilelile la miaka yote, kushika sikio lako. Wapo walioshindwa ambao walilia kama nilivyofanya miaka miwili iliyopita lakini pia walikuwepo wale waliofaulu na kutakiwa kujiunga na shule hiyo kwa ajili ya kuanza na elimu ya msingi huku nikiwa nimeandikishwa jina jingine na kuitwa Bahati. 
AANZA MASOMO
 Niliipenda masomo, niliipenda shule kwa jinsi majengo yake yalivyokuwa. Yalipendeza na kuvutia sana. Siku hiyohiyo ambayo baba alikuwa amenipeleka shuleni hapo, tukaingizwa darasani na kupangwa, siku iliyofuata, tukaanza masomo huku tukiwa watoto zaidi ya arobaini katika darasa moja. Kila mmoja alionekana kuwa na furaha kama nilivyokuwa. Hakukuwa na utulivu, kila wakati wanafunzi walikuwa wakipiga kelele, nadhani kwa walimu au kwa watu waliokuwa katika mitaa yenye watoto wengi watakuwa wanalitambua hili, jinsi watoto wanavyopiga kelele zenye kuleta kero.
 AONGOZA KWA UTUNDU
 Kati ya wanafunzi wote waliokuwa darasani, mimi ndiye nilionekana kuwa mtundu. Kwanza sikutulia sehemu moja, nilionekana kama mtu aliyekuwa akitafuta kitu fulani, muda huu unaweza kuniona hapa na baadaye kuniona kule. 
UTUNDU WAMPA UMONITA
 Kutokana na utundu wangu wa muda mfupi, hata mwalimu wa darasa hilo aitwaye Rugemilila alipoingia darasani, akanichagua niwe ‘monita’ yaani kiongozi wa darasa lile. Maisha ya nyumbani yaliendelea kuwa vilevile kwamba kila nilipokuwa nikirudi na kula chakula, mama alinitaka nioshe vyombo. Bado mama alinifundisha mambo mengi huku akitamani sana niwe kama wasichana wengine, nadhani mbele ya maisha yangu aliyaona kwani kwa kile alichokuwa akikitaka ndicho kimeweza kunisaidia sana kipindi hiki.
 AKAMUA NG’OMBE MAZIWA
 Kazi zote za nyumbani ambazo alikuwa akizifanya mama, ilikuwa ni lazima na mimi nizifanye. Siku ambayo sikuwa nikienda shule, ilikuwa ni lazima nipike japo chai na kufanya usafi nyumbani hapo huku nikisaidiana naye. Nyumbani kulikuwa na ng’ombe, kila siku, hata kabla ya kwenda shule ilikuwa ni lazima niamke asubuhi sana, nikamue maziwa na kisha mtu ambaye alikuwa akihusika kwa ajili ya kwenda kuwachunga akiwatoa zizini na kwenda nao machungoni.
 ACHUNGA NG’OMBE
 Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu ya kila siku. Siku ambazo sikuwa nikielekea shuleni, pia nilikuwa nikichukuliwa na kupelekwa machungoni. Nilichukia kazi nyingine lakini hii ya kuwapeleka ng’ombe machungoni niliipenda kwa sababu ilinipa nafasi ya kuondoka nyumbani hapo kwenda kuzurura na ng’ombe hao.
 AUZA CHIPSI
 Kutokana na utundu niliokuwa nao na ujanja wa hapa na pale, mwalimu wangu wa darasa akanichagua niuze chipsi zake. Wanafunzi wengi walikuwa wakiitamani kazi hii kwani walijua fika kwamba mara unapouza na nyingine kubaki, walimu huwa na kawaida ya kukupa mfuko mmoja ule.
Chanzo-globalpublishers


No comments:

Post a Comment